TBL yafuta ajira 100...

TBL yafuta ajira 100...


KAMPUNI ya Bia ya Tanzania Breweries (TBL), imepunguza watumishi wake takribani 100 ndani ya saa 24.

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata kutoka kwa watumishi wa TBL, zinadai kwamba watumishi waliopunguzwa ni wale wa kitengo cha masoko.

Mtoa taarifa mmoja kutoka kwenye duru za uongozi wa TBL ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini, ameliambia gazeti hili kuwa uamuzi huo ulitekelezwa Jumatatu ya wiki hii.

Alisema sababu kuu ya kupunguza wafanyakazi hao ni kulinda uchumi wa kampuni baada ya mauzo ya bidhaa kuporomoka kwa kasi katika kipindi cha mwaka jana hadi mwaka huu.

Ofisa masoko mmoja wa kampuni hiyo ambaye hajakumbwa na panga la kupunguzwa kazi, alidokeza kwamba uamuzi huo unatokana na hali ya mauzo na uchumi wa kampuni kutokuwa rafiki.

Aliongeza kuwa uamuzi wa Serikali wa kuzuia biashara ya pombe kali zinazofungashwa kwenye mifuko ya plastiki(viroba) umeathiri kwa kiasi kikubwa soko la bidhaa yao aina ya Konyagi.

“ Wameachishwa kinyama sana, waliitwa siku ya Jumatatu na kuachishwa papo hapo(on spot), wakaambiwa wayaache magari yao na kusaini fomu ya kuondoka, miye kwa bahati nzuri  nimepona. Na hili jambo la viroba ndio limepigilia msumali wa mwisho,” alisema ofisa huyo.

MTANZANIA Jumamosi lilimtafuta kwa njia ya simu, Msemaji wa Kampuni ya TBL, Georgia Mutagahwa kwa ajili ya uthibitisho wa taarifa hiyo, hakupokea simu kila ilipopigiwa lakini akatuma ujumbe mfupi kuwa kabanwa na majukumu hivyo akaomba aandikiwe ujumbe mfupi wa maandishi.

Alipoandikiwa ujumbe mfupi wa maandishi juu ya madai hayo hakujibu na hata alipopigiwa tena hakupokea simu.

Kuuzwa kwa TBL

Kumekuwa na hali ya sintofahamu juu ya uhalisia wa madai ya kwamba Serikali imeishauza hisa na mali zake za Kampuni ya TBL kwa Kampuni ya Sab Miller ya nchini Afrika Kusini.

Inaelezwa kwamba uamuzi huo uliifanya kampuni ya Sab Miller kuungana na kutengeneza faida kubwa kwa pamoja na  Kampuni ya Anheuser-Busch (AB) InBev ya nchini Ubeligiji.

Dadisi za mambo zinadai kuwa serikali ilidanganywa  na hivyo kufikia uamuzi wa kuuza kampuni ya TBL mwishoni mwa utawala wa awamu ya nne.

“ Kuna dalili ya kwamba Serikali ya Awamu ya nne ilidanganywa kuuza hisa zake mutalab za viwanda vya bia cha TBL  na mali nyingine kwa ujumla wake kwa lengo la kupata fedha lakini matokeo yake ni kujikaanga yenyewe kwa sababu iliuza TBL kirahisi na kukosa fedha nyingi kama ingekuwa na subira kuhusu mpango huo,” kiliwahi kudokeza chanzo kimoja toka serikalini.

Duru za mambo katika mifumo ya kiuchumi zinadai kuwa katika kipindi cha mwisho wa awamu ya nne, kama serikali  ingekuwa kikwazo kwa uuzaji wa kila kitu kwa  Sab Millier ya Afrika Kusini, kungekwamisha  kuungana na Kampuni ya Kibelgiji ya Anheuser-Busch  (AB) na InBev.    

Inasemekana Sab Miller inamiliki hisa zaidi ya  asilimia 57.5  za TBL  na hivyo ndio mwenye hisa nyingi zaidi ndani ya kampuni hiyo.

Wachunguzi wa biashara na uchumi wanadai kuwa serikali ilikosa uvumilivu na hivyo kuuzwa kwa hisa zake kwa bei chee.

Muunganiko (merger) hutokea pale ambapo biashara au kampuni moja inamezwa na kampuni nyingine na kupoteza utambulisho wake kwa mwenye  kuimeza na hivyo shughuli za kiuchumi huwa kubwa na hunufaika kwa ukuaji huo wa shughuli kwa kuzingatia ukubwa wake (economies of scale).

Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa  AB Inbev inamlipa Sab Miller kiasi cha dola bilioni 107 na kufanya muunganiko (merger)  huo kuwa mkubwa kuliko yote duniani  kwenye vinywaji.

Zipo taarifa ambazo hazipata kuthibitishwa na serikali kwamba uuzwaji wa kampuni hiyo ulifanywa kimyakimya kwa mauzo ya dola zinazokisiwa kuwa ni milioni 200 ambazo wakosoaji wa uchumi wanasema kuwa ni chenji tu kwani wakati huo TBL ilimethaminishwa kwa bei ya soko ya dola billioni mbili.

 



Back To Top