Mkojo wa Wema Sepetu Watikisa Mahakamani Baada ya Kukutwa na Chembe Chembe za Bangi....

Mkojo wa Wema Sepetu Watikisa Mahakamani Baada ya Kukutwa na Chembe Chembe za Bangi....



KESI inayomkabili staa wa Bongo Muvi, Wema Sepetu, jana ilichukua sura mpya baada ya mawakili wa pande mbili, ule wa utetezi na Jamhuri kuchuana kuhusu mkojo wa msanii huyo uliochukuliwa na kupimwa na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali wakati wa upelelezi wa polisi kuhusiana na mwanadada huyo kudaiwa kutumia madawa ya kulevya.Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba, shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri aliyefahamika kwa jina la Elias Mulima kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali akisoma ripoti ya uchunguzi alisema mahakamani hapo kuwa, mkojo wa Wema baada ya kupimwa ulikutwa na chembechembe za bangi.Hata hivyo, wakili wa utetezi, Peter Kibatala, alisema ripoti hiyo iliyosomwa na Mulima ina upungufu mwingi wa kisheria. Baada ya kutokea malumbano hayo Hakimu Mkazi Simba aliwaomba mawakili wa pande zote mbili kuridhia apate muda wa kuipitia taarifa hiyo ya Ofisi ya Mkemia Mkuu ili itakapoendelea aweze kuitolea ufafanuzi. Awali, kesi hiyo iliahirishwa kusikilizwa kwa muda mahakamani hapo kutokana na wakili wa Wema kutokuwepo hivyo ikaanza kusikilizwa saa 6:30. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 4, mwaka huu.Katika kesi ya msingi, Wema anatuhumiwa kukutwa na msokoto mmoja wa bangi na vipande viwili vidogo vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08. Mbali na Wema washitakiwa wengine ni wafanyakazi wake wa ndani Angelina Msigwa (21) na Matrida Abbas (16), ambapo wote wanashtakiwa kwa kosa moja la kukutwa na kiasi hicho cha dawa za kulevya. Msanii huyo na wenzake hao wako nje kwa dhamana ya wadhamini wawili waliosaini Sh. 5,000,000 kila mmoja. Inadaiwa kuwa Wema na wenzake walitenda kosa hilo Februari 4, mwaka huu, nyumbani kwake Ununio, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

 



Back To Top