Odinga Akimbilia Mahakamani Kupinga Matokeo Ya Uchaguzi...

Odinga Akimbilia Mahakamani Kupinga Matokeo Ya Uchaguzi...





Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga ametangaza kwamba muungano wake wa National Super Alliance (NASA) utawasilisha kesi mahakamani kupinga matokeo ya ushindi wa Rais mteule Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumanne ya tarehe 8 Agosti 2017 wiki iliyopita.Bw. Odinga amesema ingawa muungano huo ulikuwa umeapa kutowasilisha kesi kortini wakati huu, wameona ni heri kufanya hivyo ili kufichua uovu uliotokea wakati wa uchaguzi mkuu.“Tumeamua kwenda kortini kufichua jinsi uongozi wa kompyuta ulivyofanikisha kuiba kura zetu, “,amesema Bw Odinga akiwahutubia wanahabari jijini, Nairobi.Kiongozi huyo wa upinzani ameendelea kusisitiza msimamo wa NASA kwamba uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki huku akidai mitambo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) ilidukuliwa na matokeo kuvurugwa na kumfanya Bw Kenyatta ashinde.“Mtindo huu ulitokea pia katika maeneo mengi uchaguzi wa ugavana, Jambo kama hili halijawahi kutokea katika uchaguzi wa kidemokrasia pahala pengine popote duniani lakini ilitokea hapa“,amesema Odinga.Bw Odinga amesema udukuzi huo una uhusiano na kuuawa kwa meneja wa teknolojia katika tume hiyo Chris Msando ambaye aliuawa wiki moja kabla ya uchaguzi.Kwa upande mwingine NASA wameishutumu tume ya uchaguzi kwa kusema ilikuwa ikitangaza matokeo ya uchaguzi bila kutoa Fomu 34A za kuonesha matokeo yalivyokuwa katika vituo vya kupigia kura.NASA wamebaini udanganyifu mwingi uliotokea na kuwashutumu waangalizi wa uchaguzi ambao walisema uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki.Jamii ya kimataifa ilikuwa imehimiza upinzani, pamoja na wagombea wengine ambao hawakuwa wameridhishwa na uchaguzi, kutumia mifumo iliyowekwa kikatiba kutafuta haki.Kwa mujibu wa matokeo ya IEBC, Rais Kenyatta alipata kura 8,203,290 huku mgombea mwenza Raila Odinga akipata kura 6,762,224.

 



Back To Top