ABDUL MKEYENGE
KELELE zimekuwa nyingi redioni, mitandaoni hadi kwenye magazeti kuihusu Simba na usajili wao wa Sh. Bilioni 1.3. Kila mmoja anaandika na kuzungumza anachojisikia kuihusu Simba. Imeshachosha sasa kila siku kusikia stori za Simba kila uchwao.
Ukiwauliza mashabiki wa Simba wana maoni yao kuhusu timu na kocha wao Joseph Omog, viongozi nao wana maoni yao kuihusu timu, wanachama wana maoni yao. Simba ya Bilioni 1 ndiyo imefikia hapa katika mtego ambao wanaweza kujinasua au kuendelea kuwa na sintofahamu kubwa iliyokosa majibu stahiki.
Muda mwingi wa kelele zao nilikuwa nikijipa kazi ya ziada kutazama mapungufu ya kikosi walichonacho. Nilikitazama kikosi tena na tena na tena, kisha nikamtazama Omog nikagundua ni Haruna Niyonzima anayeleta vurugu zote hizi tunazozisikia klabuni. Na moja ya kitu kinachonogesha kelele hizi ni ubora wa Ajib kwenye jezi za Yanga. Suala hili linawauma sana watu wa Simba!
Lakini bado sijajua tatizo la Haruna linatokana na Haruna mwenyewe au Omog na majukumu anayompa uwanjani. Haruna ni mchezaji mahiri ambaye kila timu ingependa kuwa nae kikosini. Tulipoona zile picha za mashabiki wa Yanga wakipiga moto jezi zake hawakuwa wajinga, wanajua wamepoteza mwanadamu wa namna gani kikosini mwao.
Ndani ya jezi za Simba Haruna amekutana na tatizo moja. Bado anaonekana ni Haruna yule yule wa siku zote mwenye tabia ya kuuamlisha mpira na mpira kumtii bila wasi, lakini katika jezi za Simba anaonekana kutumia muda mwingi kuzunguka uwanja mzima na kusahau majukumu yake ya kukaa nyuma ya mshambuliaji wa mwisho na kumlisha au wakati mwingine kufunga.
Ubora wa Haruna unatokana na kucheza nafasi hiyo. Lakini sasa anafanya kazi nyingi zinazomuhusu na zisizomuhusu. Nadhani kuna kitu hajakijua kuwa ndani ya Simba Okwi ndiyo mfalme. Ni Okwi anayeamlisha timu iende mbele kwa haraka au ipoe. Ni Okwi anayeweza kutoka kulia kwenda kushoto na kutoka kushoto kwenda kulia au akashuka hadi chini kwa Tshabalala kuichukua mipira. Haruna hana role hii Simba, inawezekana kivuli cha Okwi kikawa kinamtesa.
Haruna amezoea kucheza kama mchezaji huru anayekabiwa na jukumu lake kubwa kupiga pasi na timu icheze kwa style anayotaka. Alivyokuwa APR ya kwao Rwanda alikuwa mchezaji huru, alivyokuja Yanga alikuwa mchezaji huru. Hapa kwa Haruna na Okwi kuna haja ya mmoja kumuachia 'Uhuru' mwenzie.
Namba hazidanganyi. Haruna mpaka sasa hajafunga bao wala kupiga pasi ya bao. Sababu ni nyepesi tu, anaondoka sana kwenye eneo analopaswa kuwa muda mrefu na badala yake amejipa majukumu ya kuzunguka muda sana na kupaacha patupu eneo lake la shimoni analotakiwa kusimama na kulitendea haki.
Rejea kwenye mechi zote mbili za Simba na Yanga ilizocheza mpaka sasa na Mkongomani wa Yanga kung'aa. Tshishimbi aliwavuruga Simba kwenye mechi zote za Ngao ya Hisani na juzi kaja kuwavuruga tena kwenye mechi ya ligi.
Tshishimbi anayecheza kiungo wa nyuma, mtu anayepaswa kuwa nae kwa ukaribu zaidi ni namba 10 wa upinzani ambaye ni Haruna, lakini haikuwa hivi. Tshishimbi hakuwa amekutana na Haruna hata mara moja katika mipira ya kugombania, kitu ambacho si sahihi.
Mtazame Kotei juzi dhidi ya Ajib. Alipokuwa Ajib hatua chache nyuma yake alisimama Kotei. Kupenda kuzunguka muda mrefu kunamfanya Haruna aonekane kupoteza ubora na anazidisha kumpa ubora Tshishimbi.
Anachokifanya sasa Haruna ndicho alichokuwa akikifanya na Yanga, lakini Yanga hawakuwa na Okwi. Hivyo Haruna alisimama kama bosi wa Yanga uwanjani. Ni yeye aliyeamuru nani apasiwe nani asipasiwe. Kila shambulizi langoni mwa adui lilianzia kwake. Muda huu ambao yuko Simba, maisha yamekuwa tofauti kidogo.
Hata huu ubora wa Ajib hivi sasa umetokana na Yanga kutokuwa na Haruna kikosini mwao. Jiulize ni viungo wangapi Yanga walionekana wa kawaida walipomkuta Haruna? Mtafute Deus Kaseke yule wa moto aliyekuwa Mbeya City. Deus alikuwa kila kitu Mbeya City, lakini alipokuja Yanga alikuwa mtumwa wa Haruna.
Omog anapaswa kuitazama upya line up yake kuhusu eneo analopaswa kumuweka Haruna bila kuingiliana na Okwi na akapata ubora sahihi wa Haruna. Tunavyoona Haruna hajafunga wala hajatoa pasi ya bao mpaka sasa, si kama haba bahati, majukumu aliyonayo.
Njia nyingine ya Omog kumrejesha Haruna aliyezoeleka Tanzania ni kumpunguzia majukumu ya kuzunguka eneo kubwa la uwanja na kumwambia asilikimbie sana eneo lake. Haruna analindwa na Kotei, Mzamir na wakati mwingine Mkude wanaocheza nyuma yake, lakini bado anapenda kurudi deep kuifuata mipira na kulifanya eneo lake lipwae.
Hakuna link ya Haruna na wachezaji wenzie licha ya Haruna kuwa mchezaji mzuri mwenye kipaji maridhawa. Siku ambayo Haruna atapunguza kuzunguka uwanja kwa kiwango kikubwa na kuamua kufuata miiko ya namba 10 ndiyo siku ambayo wahafidhina wa Simba watasalimu amri juu ya Haruna.
Lakini kama uchezaji huu wa sasa utaendelea kuwepo siku hadi siku tunaweza kumuona Haruna kama ameisha, kumbe mchezaji anakuwa amekutana na mazingira magumu ya ufanisi wa kazi zake.
Kama kila kitu kitakataa kwa Haruna, Omog anapaswa kurudi nyuma na kutuletea Mohamed Ibrahim (MO) Said Ndemla. Hawa ni brilliant players. Wana kila aina ya pasi miguuni mwao, bado ni wapigaji wazuri wa mashuti langoni. Kazi iko kwa Omog.