Lwandamina ajipanga kusajili kisasa

Lwandamina ajipanga kusajili kisasa


WAKATI Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina akikataa kumzungumzia mshambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma, kocha huyo amesema usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao utazingatia nidhamu na uwajibikaji wa mchezaji husika.

Ngoma ambaye aliachwa Dar es Salaam kutokana na kuwa majeruhi, anadaiwa amekwenda Afrika Kusini bila ya ruhusa ya uongozi wa klabu hiyo.

Lwandamina alisema kuwa anafuatilia uwezo, tabia na uwajibikaji wa kila mchezaji ndani ya kikosi hicho kabla ya kuchukua uamuzi baada ya msimu huu kumalizika.

Mzambia huyo alisema kuwa wachezaji walioko Mwanza wako katika hali nzuri na anaamini watapambana kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mechi ya kesho dhidi ya Mbao FC.

Naye nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub 'Cannavaro' alisema kuwa wamekwenda Mwanza kwa kazi moja ya kusaka ushindi.

Beki huyo wa zamani wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) amesema kuwa wanaiheshimu Mbao kwa sababu imepanda Ligi Kuu Bara msimu huu lakini imeonyesha ushindani na kiwango cha juu katika mechi mbalimbali ambazo wamecheza.

"Kila mechi kwetu ni fainali, hii ndiyo taswira tuliyonayo katika maandalizi ya mechi zote zinazotukabili za ndani na zile za kimataifa tulizokuwa tunacheza," Cannavaro alisema.

Mabingwa hao watetezi wa Kombe la FA na Ligi Kuu Bara walitinga hayua hiyo ya nusu fainali baada ya kuwafunga Tanzania Prisons mabao 3-0 wakati Mbao FC iliwachapa Kagera Sugar magoli 2-1 kwenye mechi za hatua ya robo fainali.

 



Back To Top