Simba Wamsafishia Njia Okwi ya Kucheza ligi kuu msimu Ujao...

Simba Wamsafishia Njia Okwi ya Kucheza ligi kuu msimu Ujao...



MSHAMBULIAJI raia wa Uganda, Emmanuel Okwi, sasa amesafishiwa njia ya kutua kwenye klabu yake ya zamani ya Simba ya jijini Dar es Salaam, baada ya uongozi wa timu hiyo kueleza mipango ya kuachana na beki wake raia wa Uganda, Jjuuko Murshid, ili kutoa nafasi kwa mshambuliaji huyo.

Okwi kwa sasa anakipiga katika timu ya SC Villa ya Uganda, ambako anafanya vizuri.

Rais wa Simba, Evance Aveva, amekiri ujio wa mchezaji huyo katika kikosi cha klabu hiyo kwa ajili ya msimu ujao na kueleza kwamba, Murshid, ambaye anamaliza mkataba wake, ataondoka kwenda nchini Vietnam ambako amepata dili.

Alisema kutokana na tayari beki huyo kuwapo sokoni na kushindwa kupata huduma yake msimu ujao, wana imani nafasi hiyo itachukuliwa na Okwi.

“Ujio wa Okwi Simba hauna mashaka kabisa, hapa ni nyumbani kwake, hivyo mikakati ya kuja na kuitumikia klabu yake ya zamani ipo na msimu ujao ataonekana akiwa na jezi ya Simba,” alisema.

Aveva alisema straika huyo atachukua nafasi ya Murshid, ambaye anahitaji kuondoka, hivyo ana imani watamuuza mchezaji huyo.

Ujio wa Okwi utaimarisha safu ya ushambuliaji ya Simba, ambayo mara kadhaa kocha msaidizi wa timu hiyo, Jackson Mayanja, amekuwa akiilalamikia kutokuwa makini.

Safu ya ushambuliaji ya Simba kwa sasa inaongozwa na Laudit Mavugo, Ibrahim Ajib, Shiza Kichuya na Fredrick Blagnon.

Simba wakiwahakikishia mashabiki wao ujio wa Okwi, tayari uongozi wa timu hiyo upo katika mchakato wa kuhitaji huduma ya straika wa Yanga, Donald Ngoma.

 



Back To Top