Memo Kwa Wanandoa Wote(Nakala kwa Vijana mnaotafuta/mlio katika Uchumba...

Memo Kwa Wanandoa Wote(Nakala kwa Vijana mnaotafuta/mlio katika Uchumba...



Kabla sijaoa nilishakuwa na mafanikio flani kiuchumi na kijamii. Hayakuwa makubwa "kiviiileee" lakini "somehow" yalikuwa "convicing". Nilikuwa na biashara ya kusafirisha abiria, nikiwa ninamiliki Hiace katika njia mbalimbali (ruti) mjini Iringa. Wale waliokuwepo Iringa mjini mwaka kuanzia mwaka 2008, bila shaka wanazikumbuka Hiace zilizokuwa zimeandikwa Nyaluke Trans. Pia wakati huo nilifanikiwa kuwa na cheo cha makamu mwenyekiti wa chama cha wamiliki wa magari ya abiria mkoani Iringa(IPTA). 

Ninapoelekea kuoa kuna kitu kikatokea. Ndani ya muda mfupi nilipoteza magari yooote na mtaji wooote. Watu wengi wanajua nimewahi kumiliki magari ya abiria(Hiace), lakini sijawahi kuwaeleza wengi ya kwamba yale magari nilipoteza yote na nikabaki "choka mbaya". Leo sijapanga kueleza ni namna gani hasara hiyo ilinitokea but in short lilikuwa ni pigo "matata". Ulikuwa ni wakati mgumu sana, fikiria mwenyewe,  kutoka kuwa bosi mwenye wafanyakazi kibao (madereva, makonda) mpaka kukosa hela ya kodi ya nyumba! 

Mke wangu (wakati huo kabla hata hatujafunga ndoa, akiwa mchumba), yeye akiwa ndio kwanza katoka kuajiriwa, alifanya kazi ya ziada kuniokoa. Kwanza alikuwa ananiombea na kuni-comfort na kwa miezi takribani sita nikiwa sina "mbele wala nyuma", ndie aliekuwa ananibeba kwa kila kitu kuanzia vocha. Hiyo inaweza isiwe ishu kihivo, isipokuwa ndie mtu pekee alienisaidia nijitie moyo wa kurudi kupambana tena kibiashara. Alikuwa na maneno yake yaliyokuwa yananiinua sana, "Albert you will come back, We will go further kuliko ulipopafikia kabla hujapoteza". 

Kitu pekee ambacho sikupoteza ulikuwa ni uhusiano wangu na Mungu. Siku moja nimekaa natafakari, "Kwa nini haya yametokea?", ghafla nikasikia sauti ndani yangu Mungu akiniambia, "Nimepukutisha kila ulichokuwa nacho, ili utambue thamani ya mke niliekupa, kwa sababu ungeingia na mali zako kwenye ndoa, NIMEUPIMA MOYO WAKO NA KUONA kuwa ungempuuza, kumdharau na kutompa hadhi inayotakiwa mke wako katika mafanikio yenu". Huuu! Ghafla nikajiona nimekuwa mdogo kama piritoni. 

Enewei, ngoja nisirefushe stori, lakini baadae Mungu alinisaidia, nikiwa bega kwa bega na yeye (mke wangu) tukafanikiwa na tumeendelea kufanikiwa, kumiliki thamani mara dufu ya yale magari na mtaji nilioupoteza. Kila ninachomiliki sasa, asilimia 100 kina mkono wa mke wangu. Kuna "shule" ya ajabu ambayo Mungu alinifundisha ambayo mpaka leo imenifanya niwe na heshima kwa mke wangu na niwe na adabu katika ndoa. 

Ngoja nikupe pointi japo mbili tatu:-

1). Siku utakayomfanya mwenzi wako kuwa wa muhimu kuliko chochote ulichonacho ndio siku ambayo hutadiriki kumficha chochote kuanzia mshahara, mapato yako, mawasiliano yako, na mipango yako. Ukiona uko kwenye ndoa halafu mwenzi wako hajui mshahara wako wala mapato yako, ujue kuna mahali pana ufa na hata kama unauchukulia poa leo, kuna siku utabomoa ukuta wa ndoa. Binafsi nilikuwa na akili flani hivi ya kutegemea mke aje awe ananiogopa kwa ajili ya mafanikio yangu. Ni kama nilikuwa na kiburi cha mafanikio mbele ya ndoa. Kilichotokea, "Mungu akaninyoosha ile mbaya".

2). Ukitaka uende sawa katika mipango ya ndoa, hakikisha hauweki mali na mafanikio yeyote moyoni mwako. Moyoni akae mwenzi wako sio elimu yako, sio cheo chako, sio miradi yako, sio hela zako. Mnyoosho nilioupata mpaka leo umenifanya nifike mahali ambapo moyo wangu hautembei na mali yeyote. Yaani kila nilichonacho ninakihesabu ni cha mke wangu na kwamba hata siku vikiwa havipo, mradi nibakiwe na akili na Mungu, basi nitavirejesha na kuzidi. By the way, nimethibitisha kwamba ukimshirikisha mke kikamilifu katika mipango yote ya familia, kunakuwa na spidi kubwa sana ya maendeleo.  

3). Vijana ambao bado hamjaoa wala kuolewa, na wakati huo huo mko bize kuhakikisha mnakuwa vizuri kiuchumi kabla hamjaingia kwenye ndoa, nawashauri muikague mioyo yenu. Kama mtaingia kwenye ndoa na akili za "hiki changu", "kile chake", ninawaonya mrekebishe. Tumieni makosa yangu kujifunza, hamna sababu ya kurudia makosa.
 



Back To Top