Usiku wa manane nimeamka. Katikati ya msitu mkubwa, hifadhi ya Mikumi, nasikia sauti za ndege na wanyama wengineo wakilia mwituni. Watoto wamelala fofofo.
Nimeshtuka ghafla usingizini. Natafakari tukio kubwa la lililotokea jana Juni 19, 2017 la kukamatwa kwa ndugu Harbinder Singh Seth, mmiliki wa kampuni ya Pan Africa Power Solution (PAP) aliyetwaa kitapeli hisa 70% za kampuni ya kufua Umeme ya IPTL na kuchota zaidi ya shilingi 306 bilioni kutoka Benki Kuu ya Tanzania.
Navuta picha ya mahakamani, namwona pia ndugu James Rugemalira mmiliki wa hisa 30% za IPTL, na aliyeuza hisa hizo kwa ndugu Seth kwa malipo yaliyotokana na fedha zilizoporwa kutoka Benki ya Tanzania (BOT). Picha ya watu hawa wakiwa mahakamani chini ya ulinzi wa polisi ilinipeleka mbali Sana kimawazo.
Nakumbuka ujumbe mfupi wa simu (SMS) wa ndugu Richard Mgamba wa Februari 2014, aliyeniandika "piga". Nilikuwa Washington DC nchini Marekani wakati huo, najivuta kupiga simu maana gharama ni kubwa kupiga simu kutoka Marekani.
Napiga simu kwa ndugu Mgamba, ananiwahi kwa swali hata kabla ya salaam "POAC mlizuia fedha kwenye Escrow zisitoke, unajua zimetoka? Tunataka kuandika", ananiuliza. Wakati huo Richard Mgamba alikuwa ni Mhariri wa Habari za Uchunguzi wa gazeti la The Citizen.
Namuomba anipe muda nihakiki taarifa anazonipa. Napiga simu mbili tatu kwa watu mbalimbali kwenye taasisi za Serikali na kuthibitisha. Nikarudi Kumjibu Richard "Ni Kweli endelea. Nyaraka nikirudi".
Wiki hiyo gazeti la The Citizen wakaandika Habari ile kwa mara ya kwanza. Nilikuwa London wiki ya mwisho ya February 2014, wakati Kampuni ya PAP ilipoanza kutoa vitisho na kufungua kesi dhidi ya The Citizen. Nikawa nimerudi nchini na kuanza kukusanya nyaraka muhimu ili kuwasaidia The Citizen.
Naenda kumwona ndugu Ludovick Utouh, aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Yeye na timu yake walikuwa katika ukumbi wa Hoteli ya Giraffe, Mbezi Beach, jijini Dar es salaam wakiandika Taarifa ya mwaka ya Mahesabu ya Serikali, Taarifa yake ya mwisho akiwa CAG.
Nikiwa namsubiri Mzee Utouh hotelini hapo, msaidizi wake ananijulisha kuwa amepata kikao ghafla Wizara ya Nishati na Madini, kuzungumza na Katibu Mkuu wa Wizara, ndugu Eliakim Maswi, pamoja na Mwanasheria wa Wizara Dkt. Medard Kalemani.
Hivyo naendelea kumsubiri, baada ya nusu saa Utouh anakuja. Namwambia "nimetoka kuonana na (namtajia jina na cheo - kwa sasa nalitunza si vema kumtaja), amenipa nyaraka zote za fedha zilizotunzwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow na kutolewa kulipwa PAP kama mmiliki wa IPTL. Sisi PAC tunataka sasa ufanye ukaguzi maalumu wa suala hili".
Nikiwa London nilikuwa nimeshampigia simu mzee Utouh kumwambia asome gazeti la The Citizen. Pia nilikuwa nimezungumza na Makamu Mwenyekiti wa PAC, ndugu Deo Fulikunjombe juu ya jambo hili. Yeye baada ya kushauriana na wajumbe wa Kamati tulikubaliana kuwa njia bora ni hiyo ya uchunguzi wa CAG.
Katika mazungumzo yetu Mzee Utouh ananiambia kuwa alikuwa na kikao na Maswi na ameomba pia ukaguzi maalumu. Nikashtuka kidogo maana anayeagiza ukaguzi maalumu ndiye anapewa Taarifa hiyo. Nikajua nini cha kufanya.
Nilimaliza kikao saa nne usiku na kumfuata kwanza ndugu Mgamba na kumpa nyaraka kadhaa muhimu ambazo nilizikusanya baada ya kurudi nchini (kujihami iwapo nitavamiwa na kupoteza nyaraka husika). Nikampa nakala nyengine msaidizi wangu ili ziwe scanned na kuwekwa www.jamiiforums.com, kisha nikafanya kikao cha dharura na ndugu Deo Filikunjombe.
Tukakubaliana Deo awasiliane na Spika kumwomba idhini ya kikao cha dharura cha PAC, na Mimi niwasiliane na Katibu wa Bunge kuwaambia makatibu waitishe kikao. Baada ya siku mbili tukamwita Gavana wa Benki Kuu mjini Dodoma. Baada ya kikao kifupi PAC ikaagiza rasmi ukaguzi Maalumu kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow. Tukaagiza Taarifa iletwe Bungeni na sio Wizarani.
Mkakati huu ulitusaidia mno mbeleni kwani juhudi za Serikali kuzuia ukaguzi ziligonga mwamba maana mchezo wa Wizara tuliushtukia na kuuzuia. PAC ilitoa Taarifa kwa Umma juu ya ukaguzi husika, lakini ni The Citizen peke yake waliotoa habari ile.
Tulishindwa vita ya habari mapema sana kiasi cha taarifa rasmi za PAC kutoandikwa kabisa. Mwezi Machi nikapata jukumu la mtoto kwa mzazi ambapo mama yangu aliumwa ghafla na ikapaswa nimpeleke kwenye matibabu India. Alikuwa mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na hivyo Bunge kulipia gharama zake za matibabu.
Hii maana yake ni kwamba sikuwa na muda wa kufuatilia suala hili, hivyo ilibidi kumpa nguvu Makamu wangu aliyebaki kuendesha Kamati ya PAC, namshukuru sana ndugu yangu Deo Fulikunjombe kwa uzalendo wake, alifanya kazi kubwa sana.
Mungu akasaidia sana, ndugu David Kafulila akajitokeza kubeba jukumu la kuweka shinikizo kwa Serikali. Yeye akitaka Kamati Teule ya Bunge yenye kuundwa na Wabunge kuchunguza suala hili. Aliongea kwenye Makadirio ya Ofisi ya Waziri Mkuu mwezi Aprili na akaendelea kuibua jambo hili kila alipopata nafasi.
Mwanzoni magazeti mengi yalikuwa yanapotezea habari hii, na hata michango ya Kafulila. Nakumbuka baada ya hotuba ya Waziri Mkuu niliwaambia wahariri kuwa wamevaa miwani za mbao. Kafulila hakuchoka akaendelea kusema kila aliposimama Bungeni hali iliyopelekea aitwe Tumbili.
Tulipata msaada pia wa aliyekuwa Mbunge wa Simanjiro, ndugu Chritopher Ole Sendeka, alitoa msaada mkubwa sana kwa kamati. Naye akatukanwa kuwa hakuwa msomi na alipata zero akiwa kidato cha sita. Vyombo vya Habari vilishangilia sana vioja hivi vya Waziri kutaja matokeo ya shule ya mbunge bungeni ili kumvunjia heshima mbele ya jamii.
Mtindo huu wa kuvunjia watu heshima pia ulitumika dhidi yangu, kwa kutengeneza kijitabu cha propaganda kilichogawanywa kwa ustadi na mafanikio makubwa kwa kila Mbunge nyumbani kwake mjini Dodoma. Kijitabu hicho kilijaa uzushi kwamba nimehongwa na ndugu Seth wa PAP na mambo mengine mengi ya kutia aibu. Kukumbuka tu haya kunatia uchungu mno, na ninavuta hisia za waliotengeneza vijitabu vile na kusambaza na waliowalipa. Inasikitisha sana nikikumbuka haya.
Ilibidi kuingia kwenye kuandika makala kwenye magazeti ili kuwaelimisha wananchi kuwa fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow zilikuwamo za Umma. Seth akaamua kutushitaki mimi pamoja na gazeti la Raia Mwema kwa kuchapisha makala husika, na kutudai shilingi 500 bilioni. Kesi husika inaendelea mpaka Leo mahakamani.
Magazeti mengi yalianza kuimba wimbo wa Seth. Jamii iligawanyika sana kwani PAP na Seth walianza kutoa misaada kwenye nyumba mbalimbali za ibada pamoja na taasisi za Serikali kama Jeshi la Polisi. Tulivunjwa moyo mno katika mazingira yale, lakini hatukukata tamaa.
Ilibidi niandae andiko maalumu kuelewesha jamii ya wasomi kuwa Seth na wenzake ni matapeli. Kupitia mawakili wa kimkakati tulipata nyaraka za kuonyesha kuwa Seth alipewa hisa za IPTL bila kulipa kodi ya ongezeko za mtaji.
Wakati mwengine mambo hutokea duniani kwa mipango ya mungu. Mwaka 2012 nilikuwa nimepeleka Bungeni mabadiliko ya sheria za Fedha zenye kutaka kuwa uhamisho wa umiliki wa kampuni usifanyike mpaka kwanza kodi imelipwa na cheti cha kamishna wa kodi kimetolewa, lengo lilikuwa ni kuongeza mapato ya Serikali na kupunguza ukwepaji wa mapato, hasa kwenye sekta ya madini, mabadiliko hayo ni maarufu kwa jina la "Capital Gain".
Ni mabadiliko hayo ndiyo ambayo yalikuja kuwa msaada mkubwa sana kwenye harakati hizi za uchunguzi wa kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow.
Nilipomaliza andiko lile likalifasiri Kwa Kiswahili na kutengeneza kitabu maalumu. Nikakaa na David Kafulila na kutafuta fedha ili afanye ziara kwenye mikoa kadhaa, ikiwemo Mwanza na Mbeya ili kuzungumza na wananchi moja Kwa moja na kugawa kijitabu kile.
Ndugu yangu mmoja (sitamtaja kwa jina, namshukuru sana) akanisaidia usanifu na picha kwa ajili ya kijitabu kile, picha tuliyoitumia tuliipata kutoka kwa mpiga picha wa gazeti la mwananchi. Mdogo wangu mmoja, ndugu Balozi Jamanda akazalisha nakala za kutosha za kijitabu na kusambaza nchi nzima kwenye ziara za Kafulila ambazo nilizifadhili ili kuendeleza mjadala tukiwa tumesusiwa na vyombo vya habari.
Septemba 2014, nikaenda Kwa CAG kuwasilisha maelezo yangu ambayo kimsingi ilikuwa kitabu kile. Wakati huu sasa The Citizen walikuwa wamepata nguvu ya Raia Mwema chini ya Ezekiel Kamwaga na Mtanzania chini ya Dennis Msaki (kwa ushawishi mkubwa wa mwandishi kijana Freddy Azzah). Tukaanza kupata nguvu na shinikizo likaendelea.
Tukapata hati halisi za umiliki wa Mechmar kutoka benki ya Standard Chartered ya Hong Kong. Kimkakati tukaitoa hati hii kupitia gazeti la The Citizen na wakaichapisha. Tukawa tunapata uelewa wa wananchi kwa kuridhisha kabla ya CAG kuwasilisha taarifa yake kwenye Kamati.
Watu wa PAP/IPTL nao waliongeza nguvu. Sauti dhidi ya ukwapuaji ule ilikuwa ni ya Kafulila na PAC tu. Ilituvunja moyo sana kuwa viongozi wengine wa vyama vya upinzani nchini walikuwa kimya kabisa mpaka dakika za mwisho. Tulikuwa tunajiuliza nini hasa kimetokea? Tulipata nguvu ya pamoja baada ya hoja kufikishwa kwenye Kamati na Kwa makusudi kabisa kuvujisha baadhi ya taarifa kwenye vyombo vya habari ili kupata uungwaji mkono wa wananchi.
Watu wa PAP/IPTL pia walikuwa na mikakati yao ya vyombo vya Habari. Kwanza walicheza na Taarifa ya CAG na kuisambaza kwa nguvu kabla ya taarifa rasmi kutolewa. Hawakujua kuwa sisi PAC tulikuwa na tarifa ya kwanza kabisa ya CAG ambayo ilikuwa na ukweli wote kabla ya taarifa yao iliyochezewa. Ndio maana kulikuwa na mchanganyiko mkubwa Kwa umma kuhusu Fedha ni za Umma au si za Umma, kwani ilikuwa ni mkakati maalumu wa wakwapuaji wa fedha zile.
Ili kujenga umoja ndani ya Bunge nilimwomba spika kuniongezea wajumbe kwenye Kamati, ombi ambalo lilikubaliwa. Tuliongezewa wajumbe kadhaa, akiwemo ndugu Kangi Lugola, Suleiman Zedi na Dkt. Hamis Kigwangalla. Hawa walikuwa ni viongozi wa Kamati nyengine. Lengo letu lilikuwa ni kuongeza nguvu kwenye Kamati ya Uongozi na pia sauti zenye uelewa. Tulitaka kuwe na taswira kubwa ya Kamati, isiwe tu ni PAC, iwe ni ya vyama vyote na yenye taswira ya Kitaifa. Jambo hili lilitusaidia sana.
Wakwapuaji nao walijipanga kwenye Fedha. Walikuwa wanagawa fedha Kwa kila mbunge anayechangia. Sisi tuliamua kuwachezea mchezo wa kupanga wachangiaji wetu wazuri siku ya mwisho na wao wakajaa kuchangia siku ya pili ya uwasilishaji wa taarifa bungeni, alhamis. Deo Filikunjombe alifanya kazi hiyo ya mkakati.
Spika Makinda na kabla yake Naibu spika Ndugai walitupa ushirikiano mkubwa. Ndugai alitwambia wakati wa kukabidhiwa ripoti, namnukuu "waelezeni Watanzania ukweli. Nipo nanyi". Kweli alikuwa nasi na ili kutupunguza nguvu akapewa safari ya ghafla kwenda Paris. Lakini Spika Makinda alikuwa ameelewa jambo hili vizuri sana. Alitupa mwongozo kama mzazi, kutoka mwanzo mpaka mwisho. Naushukuru sana uongozi wa Bunge.
Pia tulijua kuwa wabunge wa CCM wakiweka msimamo wa kupinga, taarifa yetu itakwama. Siasa za kibunge uamuliwe kwa msingi wa Demokrasia wa "wengi wape". Wabunge wa CCM ndio wengi bungeni, ukitaka jambo lako ni lazima ujenge ushawishi kwao. Ilibidi niongee na aliyekuwa Katibu Mwenezi, ndugu Nape Nnauye akiwa kwenye ziara mikoa ya Kusini na kumwambia amwombe Katibu Mkuu wao, ndugu Abdulrahman Kinana kuwa pasiwe na msimamo wa Chama chao kwenye jambo hili. Kuwe na Uhuru wa Wabunge wa CCM kuzungumza. Ndugu Kinana akatuhakikishia hilo.
Deo Filikunjombe akazungumza na Mzee Mangula ambaye alikuwapo dodoma kumwomba hivyo hivyo. Mzee Mangula alimwuliza "kwanini maazimio umesoma wewe na sio Mwenyekiti wako? Sio mtego kuwa wewe ndio unyonge CCM wenzako?". Bahati nzuri jambo tulilipanga vizuri kabla.
Mimi nilikuwa kwenye ugomvi mkubwa na Chama changu wakati huo Chadema. Kwahiyo kwanza ilibidi nijisogeze kwao ili taarifa isipate mkwamo, lakini pia ilibidi ionekane ni kazi ya pamoja hivyo tusome Mimi na Deo ambaye alikuwa CCM. Tulifanikiwa sana. Hii ilikuwa kazi hasa ya wabunge wote, bila kujali vyama vyao, kitaswira na kwa uhalisia.
Hata Kamati ya kuandika maazimio tukawaweka watu kama ndugu Tundu Lissu na Freeman Mbowe, na upande wa CCM, ndugu Anna Kilango Malecela ambaye mwanzoni hakuwa upande wetu. Tulifanikiwa kujenga mwafaka wa kibunge.
Watafiti watakapokuwa wanaandika kuhusu 'Siasa za Bunge'watakuta kuwa huu ni mfano bora Kabisa wa kujenga mwafaka ndani ya Bunge Kwa maslahi ya Taifa. Azimio la kwanza Kabisa likawa Harbinder Singh Seth akamatwe na kushtakiwa kwa utapeli na wizi.
Jana nilipoona picha ya Seth akiwa anapandishwa mahakamani chini ya ulinzi wa polisi nikapata msisimko mkubwa Sana. Kisaikolojia picha ile ina maana kubwa sana kwenye vita dhidi ya ufisadi nchini. Rais Magufuli amefanya jambo la kiukombozi (psychological liberation).
Naamini watu Kama David Kafulila jana walikuwa na furaha sana ya kuona matunda ya kazi yao. Alisimama kidete kuhakikisha ajenda haifi mpaka PAC ilipomaliza kazi. Wajumbe wa Kamati ya PAC ya 2013 - 2015 wote wanastahili pongezi kubwa maana tungekubali kugawanywa tu tungepoteza ajenda.
Mshikamano tulioonyesha ilikuwa silaha kubwa. Wapo mashujaa ambao siwezi kutaja majina yao (Unsung Heroes), hawa ni wengi mno, wengine ni watumishi wa bunge. Sitaki kuwataja lakini vijana wale na mama yule chini ya katibu wa Bunge walipata majaribu makubwa Sana. Walisimama kidete.
Mtu mwengine muhimu kwenye jambo hili ni mzee wangu Edward Hosea wa Takukuru. Yeye, Utouh pamoja na watumishi wa Ofisi ya CAG walisaidia Kamati kwa kiwango cha juu kabisa. Mpaka Leo nikimuwaza Hosea kwenye sakata hili kama nimevaa kofia ninaivua kwa heshima kubwa sana kwake.
Aliyekuwa Kamishna wa TRA, ndugu Rished Bade alikata mzizi Wa fitina kwa kuithibitishia Kamati ya PAC ushahidi nyeti sana kuhusu masuala ya kodi. Ni ushahidi huu ambao kama tungeukosa pengine tusingekuwa na taarifa kama ile.
Bunge lilifanya kazi yake, kwa ufahari kabisa, likasaidia Taifa kwa kuleta maazimio yale yaliyolipa heshima. Naona fahari sana kuhudumu kwenye bunge lile.
Jambo hili la Tegeta Escrow limenionyesha kuwa "Watu wema hawafi, hata kama miili yao iko mchangani tayari (kaburini)", na hili ndilo linalojidhihirisha kwa ndugu yangu na rafiki yangu wa karibu mno, aliyekuwa makamu wangu wa uenyekiti wa PAC, Deo Fulikunjombe. Miaka miwili tangu afariki sasa, bado taifa linakumbushwa juu ya uzalendo wake.
Sijui Deo angekuwa hai jana angekuwa katika hali gani. Ninamlilia ndugu yangu. Kitu kimoja ambacho watu wengi hawajui ni kwamba muda wote wa kuandaa tarifa maalum ya PAC kuhusu Tegeta Escrow yeye ndiye aliandaa ulinzi wangu kuhakikisha sidhuriwi. Alimwambia dada yangu aje dodoma kuhakikisha ninakula kile tu kilichpikwa na dada yangu. Shujaa wa kazi hii ni yeye. Ingawa Mimi na yeye tulikubaliana kuwa Gazeti la The Citizen ndiye haswa lililohitaji kutambuliwa kwa kazi hii.
Bahati mbaya sana sisi wanasiasa ndio huonekana zaidi kwa sababu tuna sauti, jambo hili hufanya historia isiwataje wasio wanasiasa, ndio msingi wa waraka wangu huu, kuwapa haki yao wale wasio wanasiasa waliofanikisha kazi hii ngumu kwa maslahi ya Taifa letu.
Mhariri wa gazeti la The Citizen, ndugu Richard Mgamba na waandishi wake kama Mkinga Mkinga ndiyo mashujaa hasa wa jambo hili, kwa niaba ya wenzangu tuliokuwa kwenye Kamati ya PAC, ninawashukuru sana. Tulivunja mwiko na kwenye Taarifa ya Kamati yetu, tulitambua rasmi kazi ya chombo cha Habari katika vita dhidi ya rushwa.
Gazeti la The Citizen lilitimiza wajibu wake katika wakati ngumu Sana wa kupingwa na waandishi wenzao na hata waajiri wao. Mnastahili heshima kubwa sana. Ahsanteni sana.
Funzo kubwa muhimu katika kadhia hii yote ni umuhimu wa uhuru wa kiutendaji wa taasisi mbalimbali nchini. Taasisi huru husaidia uwajibikaji mahali penye makosa, husaidia kufichua ufisadi, na huleta uwazi. Yawezekana bila Uhuru wa Takukuru, CAG, BOT, TRA, Vyombo vya Habari pamoja na Bunge leo nisingekuwa nazungumza haya, ni muhimu sana tupiganie na kulinda uhuru huu wa taasisi.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Juni 20, 2017
Mikumi
Tanzania