Labda ‘tabia yake’ itawapa ubingwa Yanga msimu huu, si kwa mbinu za Lwandamina na Nsajigwa

Labda ‘tabia yake’ itawapa ubingwa Yanga msimu huu, si kwa mbinu za Lwandamina na Nsajigwa



Na Baraka Mbolembole
KATIKA michezo miwili waliyokusanya pointi nne mjini Njombe na Songea, timu ya Yanga haikuonekana kucheza vizuri  huku safu ya kiungo ikionekana ‘kuchemka’. Goli la mpira wa faulo lililofungwa na Ibrahim Ajib ndilo liliwapa ushindi wa kwanza msimu huu kikosi cha Mzambia, George Lwandamina vs Njombe Mji.
Sababu za hali ya hewa ya baridi huko Njombe zilichukuliwa sababu ya timu hiyo kuambulia ushindi ‘kiduchu’ wa 1-0 dhidi ya Mji Njombe ambayo ilikuwa ikicheza mchezo wake wa pili wa ligi kuu baada ya awali kufungwa 2-0 katika uwanja wa Sabasaba, Njombe na timu ya Tanzania Prisons.
Nilishangazwa sana na sababu ambazo kocha msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa alizitoa mara baada ya timu yake kupambana ‘kufa na kupona’ kusawazisha goli la Peter Mapunda wakati, Donald Ngoma alipowaepusha mabingwa hao watetezi na kipigo cha kwanza msimu huu mbele ya Majimaji FC siku ya Jumamosi iliyopita.
Nsajigwa bila ‘aibu’ alisikika akisema, ubovu wa sehemu ya kuchezea katika uwanja wa Majimaji ulichangia mchezo wa hovyo  wa timu yake, nadhani amesahau kuwa walicheza katika kiwango cha chini pia wakati walipolazimisha sare ya kufungana 1-1 na Lipuli FC katika uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam siku ya ufunguzi wa msimu.
Salvatory Edward
Katibu mkuu wa Yanga, Charles Mkwassa ni kocha-mchezaji mzuri wa zamani wa klabu hiyo. Mkwassa ni miongoni mwa makocha waliofanikiwa kiufundishaji katika soka la Tanzania. Anaweza kuwa sahihi wakati alipokubali klabu kutoongeza mkataba na aliyekuwa kocha msaidizi, Juma Mwambusi.
Kuondoka kwa Mwambusi ndiko kumempa nafasi Nsajigwa japokuwa, Lwandamina alipendekeza jina la Mecky Maxime kuwa msaidizi wake hata kabla ya kumalizika kwa mkataba wa Mwambusi na Yanga. Nsajigwa ni chaguo baya kwa wakati huu ambao timu inapitia mabadiliko makubwa ndani na nje ya uwanja.
Ukiachana na mataji manne aliyoshinda akiwa mchezaji wa Yanga (2006, 2007/08, 2008/09 na 2010/11) kiufundishaji Nsajigwa hajawahi kuonyesha uwezo wowote ule kiufundishaji na kama Yanga ilihitaji ‘mtu wao’ zaidi kuliko Maxime basi, Salvatory Edward angekuwa chaguo sahihi zaidi kwa sasa kuliko Nsajigwa.
Salva tayari ameonyesha yeye ni kocha  mwenye mbinu bora za kushambulia akiwa na kikosi cha Yanga B, pia ndiye kocha aliyeipandisha ligi kuu African Lyon miezi 15 iliyopita huku timu hiyo ikicheza mchezo wa kushambulia.
Ukitazama vikosi vya Lwandamina vile vinavyocheza tangu alipochukua timu hiyo kutoka kwa Mholland, Hans van der Pluijm utagundua kuwa timu yake haishambulii sana. Lwandamina anaonekana ni mzuri katika mbinu za kuzuia ndiyo maana hajawahi kukutana na tatizo kubwa klabuni hapo, lakini ameonekana kushindwa kutengeneza muunganiko wa timu kutoka nyuma-katikati-hadi kwa safu ya mashambulizi.
Alipomuhitaji Maxime alikuwa na maana ya kuhitaji kocha msaidizi ambaye atakuwa na mbinu bora za mashambulizi na kwa muda ambao alikuwa Tanzania na kukutana na wapinzani 15 tofauti, Lwandamina alimchagua Maxime kwa kuamini ni kocha mwenye mbinu sahihi za mashambulizi.
Nsajigwa ni mchezaji ambaye alitumia muda mwingi kiuchezaji kucheza nafasi ya ulinzi, ndiyo hata Maxime alikuwa mlinzi wa pembeni lakini mtazamo wake katika mashambulizi ulikuwa wa kiwango cha juu kuliko Nsajigwa.
Inawezekana Maxime hakuwa tayari kuacha kazi Kagera Sugar FC na kwenda kuwa msaidizi wa Lwandamina lakini kitendo cha kocha huyo bora wa ligi kuu msimu uliopita kukubali kukaa meza moja na Yanga ilikuwa dalili ya kuonesha yuko tayari. Sijui ilikuwaje ikashindikana.
Naamini, Nsajigwa ni chaguo la ungozi lakini nao kwa manufaa ya timu wangepaswa kumchukua Salvatory ambaye angeweza kumsaidia Lwandamina namna ya kuunganisha kikosi na timu kucheza katika muonekano wa kitimu kama wakati ule wa Hans. Yanga ina kikosi kizuri lakini wachezaji wake wamekuwa wakiporomoka viwango huku timu ikicheza hovyo.
Kwanini Buswita hachezi?
Kuondoka kwa Haruna Niyonzima, Deus Kaseke na Saimon Msuva katika kiungo cha Yanga hakuwezi kuwa tatizo, lakini ikiwa Rafael Daud, Papy Tshishimbi, Pius Buswita na Baruani Akilimali watashindwa kufikia malengo yaliyopelekea wakasajiliwa na kocha Lwandamina.
Lwandamina  anatakiwa kuimarisha safu yake ya kiungo na uongozi unapaswa kumsaidia kwa kuhakikisha suala la Pius Buswita likimalizika ili mchezaji huyo aanze kucheza. Rafael anaingia taratibu katika mchezo wa Yanga lakini kasi yake ya kusukuma mashambulizi mbele imekuwa si nzuri.
Buswita alionesha kucheza mchezo wa kushambulia sana akiwa Mbao FC msimu uliopita. Huyu anaweza kuwa tumaini la mwisho kwa kocha Lwandamina kwa sababu wachezaji kama Said Juma Makapu na Juma Mahadhi wanaonekana kushindwa kuleta kitu tofauti hasa inapotokea Thaban Kamusoko kutokuwepo mchezoni.
Yanga wailipe haraka Simba kama wanahitaji kuona kikosi chao kikinyanyuka. Buswita anaweza kurahisha mipira kwa washambuliaji ambao licha ya timu kushindwa kutengeneza nafasi za magoli wamefunga goli katika kila mchezo. Ngoma alifunga vs Lipuli na Majimaji wakati Ajib alifunga dhidi ya Njombe Mji FC hii inamaanisha safu hiyo ya mashambulizi bado haijalala.
http://go.ad2up.com/afu.php?id=1223048

 



Back To Top